Watoto wa mitaani ni watoto wanaotangatanga mitaani kutokana na kukosa eneo maalumu la kuishi kutokana na sababu mbalimbali za kimaisha kama vile kutelekezwa, vifo vya wazazi na walezi husika pia na hali ngumu ya maisha katika jamii zetu. Mara nyingi watoto hawa hupatikana kwa wingi maeneo ya mijini kama vile Dar-es salaam, Morogoro, Mtwara, Mwanza, na Mbeya kwa sababu maeneo haya hupatikana fursa mbalimbali ambazo hupelekea kupata chochote kitu hatimaye siku zinaenda.

Sababu zinazopelekea ongezeko la watoto wa mitaani hususani nchini Tanzania, kuna sababu kadha wa kadha hupelekea ongezeko kubwa la watoto wa mitaani nchini kama vile:

  1. Hali ngumu ya maisha, kutokana na kupanda kwa gharama za maisha hapa nchini huchangia kwa kiasi kikubwa suala la ongezeko la watoto wa mitaani hapa nchini, kwani vijana wengi walisha jiingiza katika mahusiano kama mke na mume katika umri mdogo ila mara baada ya kuona hali ya maisha siyo nzuri wakaamua kutelekeza familia hatimaye watoto kukosa mahitaji ya msingi kama malazi, chakula na mavazi hivyo kuamua kujitafutia wao wenyewe.
  2. Migogoro katika jamii mfano uvunjifu wa ndoa, pia kutokana na suala la migogoro huchangia kwa kiasi kikubwa suala la ongezeko la watoto hao katika jamii zetu hapa nchini, kwani wengi miongoni mwa wanandoa pindi wakitarikiana jukumu la kutunza familia huwa wanarushiana kila mmoja hupendelea mwenza wake abebe jukumu la kutunza familia.
  3. Vifo mfano Baba na Mama, pia kutokana na ukosefu wa wazazi hupelekea watoto kutangatanga huku na kule kutafuta msaada kwa ajili ya kupata hifadhi,na huduma nyingine muhimu ambazo mtoto anastahili kuzipata ili aweze kukua vizuri na awe na afya bora badala yake endapo akikosa hukimbilia mjini kama alikuwa kijijini kwa malengo ya kujitafutia kazi mbalimbali ili aweze kukidhi mahitaji yake ya kila siku.
  4. Mmomonyoko wa maadili katika jamii mfano ongezeko la vitendo vya uzinzi, pia kutokana na suala hili huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watoto wa mitaani kwani vijana wengi hujihusisha katika masuala ya kimahusiano bila kuwa na elimu yoyote kuhusu suala hili jambo ambalo hupelekea mimba za utotoni na hatimaye hupelekea ongezeko la watoto wa mitaani hapa nchini.

Nini kifanyike ili kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani hapa nchini, ili tuweze kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani hapa nchini hatuna budi kijidhatiti katika mambo yafuatayo:

  1. Serikali haina budi kutunga sheria na kusimamia ipasavyo juu ya watoto wa mitaani, kutokana na suala hili kuonekana sugu katika jamii zetu ni lazima sheria zifuate mkondo wake kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kujenga na kukuza kizazi bora kwa manufaa ya leo na siku zijazo.
  2. Serikali, mashirika binafsi na mtu mmoja mmoja lazima tushirikiane na tuwe mstari wa mbele ili kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, kwa kuwakusanya katika vituo maalum kwa lengo la kuwapatia elimu na mafunzo, stadi mbalimbali kwani kupitia wao tunaweza kupata wataalamu kadha wa kadha kama vile mainjinia, madaktari na walimu.
  3. Jamii ipewe elimu juu ya athari za ongezeko la watoto wa mitaani katika jamii hususani elimu ya kijinsia, endapo elimu ikitolewa katika jamii wazazi na walezi watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha vijana wanafuata mambo mema na kuachana na maovu kama vile uzinzi.

Hivyo ili kuweza kupunguza tatizo hili serikali na jamii kwa ujumla bila kusahau mashirika binafsi, hatuna budi kutilia mkazo suala hili ili kujenga jamii mpya yenye muono chanya ili tuweze kufanikisha malengo na mipango mbalimbali katika jamii na hatimaye taifa kwa ujumla.

Tags:
About Author: Shaibu Namnimuka