Wanyama pori ni miongoni mwa rasilimali muhimu na bora kwa maendeleo ya uchumi katika jamii na taifa kwa ujumla endepo watatunzwa na kulindwa vizuri dhidi ya majangiri ambao huwa wanawaua wanyama hawa kwa lengo la kujipatia kipato wao binafsi pasipo kuzingatia maslahi ya jamii na taifa kiujumla, kwa mujibu wa habari na takwimu zinaonyesha kuwa wanyama wanaozidi kupungua kila uchao ni tembo na faru hususani nchini Tanzania hii ni kutokana na hitaji kubwa la mali ghafi zitokanazo na wanyama hawa kama vile pembe, meno na kwato .

Umuhimu wa wanyama pori katika maendeleo ya uchumi kijamii na taifa pia, kupitia wanyama hawa jamii na taifa hunufaika kwa minajiri kadha wa kadha kama vile:

  1. Hupelekea kukua kwa biashara katika jamii, hii ni kutokana na ongezeko la watalii mbalimbali kutoka sehemu tofauti tofauti duniani kuja nchini kwa lengo la kujionea wanyama hawa wao wenyewe hivyo basi kutokana na hitaji la malazi, chakula na hata mavazi pia hupelekea baadhi ya watu kuwekeza katika Nyanja hizo kwa lengo la kujipatia kipato chao halali.
  2. Pili, hupelekea ongezeko na upatikanaji wa ajira kwa watu mfano wakalimani, madereva na wapishi , hii ni kutokana na ujio wa watu mbalimbali katika hifadhi za wanyama kwani miongoni mwa watalii hutoka nje ya nchi mbali na hao hata wale wa ndani lazima waambatane na wazoefu ili waweze kujifunza na kutembea kwa usalama kwani watu hawa ni wazoefu wa mazingira.
  3. Tatu, kupitia wanyama pori huchangia ongezeko la pato la nchi, kupitia sekta ya utalii serikali huweza kukusanya mapato kwa mfumo wa kodi zilipwazo na watalii pindi waingiapo nchini na wale wa ndani ya nchi kwa lengo la kujifunza, kuburudika na hata kupumzika.

Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuhakikisha wanyama pori wanakuwa salama kwa manufaa ya sasa na kizazi kijacho katika jamii na taifa kiujumla kama ni yafuatayo hapa chini:

  1. Ulinzi shirikishi baina ya wananchi na serikali hususani kupitia vyombo vya dola kama vile polisi, kupitia ulinzi shirikishi utapelekea matokeo chanya kwani watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili wapo katika jamii zetu na tunajuana hivyo basi hatunabudi kuwavumbua watu hawa kwa manufaa yetu sasa na kwa kizazi kijacho hapo baadae.
  2. Kuweka wazi mapato yatokanayo na sekta ya utalii kwa umma, kwa kutumia njia hii itasaidia watu kuelewa umuhimu wa kuwahifadhi wanyama pori kwani kuna baadhi ya watu hudhania ya kwamba mali au rasilimali hii hunufaika watu wachache ndio maana huwa wanafumbia macho baadhi ya vitendo vibaya vitokeavyo kwa wanyama wetu hapa nchini.
  3. Kusimamia katika usahihi wake sheria zilizotungwa dhidi ya majangili pasipo kupendelea mtu aidha kutokana na wadhifa wake katika jamii na taifa kwa ujumla, pia endapo sheria zitafuatwa vilivyo wanyama wetu watakuwa salama hatimaye kupata manufaa makubwa sana katika jamii na taifa pia, kama vile kuboreshwa kwa miundo mbinu, huduma za jamii mfano maji, afya na mawasiliano.

Hivyo basi ili tuweze kupiga hatua katika sekta ya utalii hatuna budi kuongeza jitihada za makusudi katika kuhakikisha hifadhi zetu za wanyama pori zinakuwa salama muda wote dhidi ya majangili ambao wamekuwa kikwazo dhidi ya wanyama wetu hali inayopelekea kushuka kwa mapato yatokanayo na sekta hii kila uchao.

Tags:
About Author: Shaibu Namnimuka