Maji ni sehemu muhimu kwa kila kiumbe kilicho hai. Hakuna kiumbe kinachoweza kuendelea kuishi bila ya maji. Hii ni kwa sababu maji yana umuhimu mkubwa katika miili ya viumbe hai, hata hivyo makala hii itaangalia umuhimu wa maji kwa binadamu. Robo tatu (3/4) ya mwili wa binadamu ni maji na hii ndio sababu pekee inayoyafanya maji yawe muhimu katika mwili wa binadamu. Hivyo umuhimu huo hutokana na kazi nyeti za maji mwilini kama ifuatavyo.

1.Maji ni muhimu kwa ajili ya uhai wa seli
Kila kiumbe hai ameundwa na seli. Binadamu ana mamilioni ya seli katika mwili wake ambayo hufanya kazi mbalimbali zinazomwezesha yeye kuishi. Seli zikikosa maji hufa na hivyo kusababisha matatizo na hata kifo kwa binadamu.

2. Maji yanawezesha ufanyikaji wa michakato ya kikemikali mwilini
Kuna michakato mbalimbali mwilini mwa binaadamu inayoendelea ambayo hutegemea maji ili iweze kufanyika. Michakato hiyo ni kama vile, Usagaji wa chakula n.k.

3. Maji huwezesha utoaji taka mwilini
Kutokana na michakato mabalimbali inayoendelea katika mwili wa binadamu, takamwili nyingi huzalishwa. Takamwili hizi ni sumu na iwapo zitaendelea kuwepo mwilini huweza kuleta madhara na hata kifo. Hivyo takamwili huondolewa kwa msaada mkubwa wa maji kupitia mkojo, jasho n.k.

4. Maji ni sehemu ya damu
Takribani 52% ya damu ni maji. Maji yamechukua nafasi kubwa ya damu na hivyo kuipa tabia yake ya kimiminika. Maji huiwezesha damu itiririke kiurahisi kupitia mirija yake na kuzifikia sehemu zote mwilini.

5. Maji huipa ngozi muonekano bora
Kutokana na kazi ya maji katika tishu mbalimbali za mwili ikiwamo tishu zinazopatikana katika ngozi huifanya ngozi ionekane safi, imara na yenye afya. Upungufu wa maji mwilini huifanya ngozi isinyae na kupoteza muonekano wake.

Hata hivyo ni pale tu tutakapokunywa maji safi ndipo tunaweza kufaidika na Maji.
Lakini iwapo mtu atakunywa maji yasiyo safi na salama huweza kumletea madhara mabalimbali ikiwemo kipindupindu, Kichocho, Taifodi n.k
Ni yapi maji safi na salama?
Maji safi na salama ni maji ambayo yameepukana na uchafu na vijidudu vya maradhi kama vile bacteria.

Maji salama yanapatikana wapi?
1.Maji yanayouzwa madukani yaliyopitia viwandani na kuhifadhiwa katika vyombo maalumu ni maji safi na salama.

2.Maji yaliyochemshwa na kuchujwa, Ili kuhakikisha maji yawe safi na salama ni lazima yachemshwe na kuchujwa kwa kitambaa/kifaa kilicho safi.
Umuhimu wa kuchemsha maji ni ili kuua vijidudu ambavyo vinaweza kuleta magonjwa. Na umuhimu wa kuchuja ni kuondoa uchafu uliopo kwenye maji na hivyo kuyafanya maji yawe safi na salama.

3.Maji ya mvua
Maji ya mvua ni aina nyingine ya maji safi na salama. Hata hivyo kwa siku hizi kutokana na Uchafuzi wa hewa unaoendelea, maji ya mvua yamekuwa hatarishi na si salama kama ilivyo miaka 50 iliyopita. Hivyo ni vizuri kuyachemsha na kuyachuja kwa ajili ya kujihakikishia usalama zaidi.

4.Maji ya chemchem
Maji ya chemchem yanayotoka ardhini mara zote huwa safi na salama. Hata hivyo kutokana na matumizi makubwa ya mbolea za kikemikali ardhini, maji ya ardhini huweza kuchafuliwa. Hivyo tahadhari ichukuliwe ili kuhakikisha usalama.

Ushauri: Tunatakiwa kuchukua tahadhari juu ya matumizi ya maji ili tusije kudhurika na maji yasiyo safi na salama. Vilevile kuzingitia usafi wa vyombo vya kutunzia maji na hatua nyingine ya tahadhari hiyo.

Tags:
About Author: Abdallah Hemedi