Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vijidudu viitwavyo plasmodia.Vijidudu vya malaria vikiingia katika mwili wa binadamu huelekea kwenye ini ambako huzaliana na baadaye hujitawanya mwili mzima kupitia mzunguko wa damu. Malaria ni ugonjwa unaoweza kusababisha kifo kama mgonjwa hakupatiwa matibabu mapema.
Ugonjwa wa malaria hupatikana katika baadhi ya maeneo tu duniani. Maeneo ambayo ugonjwa huu upo ni nchi zilizizopo kusini mwa jangwa la sahara (Afrika), Amerika ya kusini na ya kati, baadhi ya sehemu ya bara la Asia na baadhi ya visiwa vya Pasifiki.

Kuenea kwa malaria
Ugonjwa wa malaria huenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine na mbu jike aina ya anofelesi. Mbu aina ya anofelesi huuma wakati wa usiku tu, na hii ndio sababu kubwa inayokifanya chandarua kiwe na umuhimu mkubwa wa kutumika wakati wa kulala ili kuzuia malaria. Pia ugonjwa wa malaria huweza kuambukizwa kwa kuongezewa damu yenye vijidudu vinavyosababisha malaria au kushirikiana sindano na mgonjwa ingawa ni mara chache sana hutokea. Mtu anapoumwa na mbu wa aina hii na akaachiwa vijidudu vinavyosababisha malaria anaweza kuanza kuoana dalili za kuugua ndani ya siku 7 hadi 16. Dalili pia zinaweza kujitokeza kabla au baada ya siku zilizotajwa kulingana na hali ya mwili ulioambukizwa.

Dalili za malaria

 • Homa
 • Kutokwa na jasho jingi
 • Baridi inayoambatana na kutetemeka
 • Kichefuchefu na kutapika
 • Maumivu ya misuli
 • Kupoteza hamu ya kula
 • Kuzimia, ikiwa malaria imepanda kichwani mgonjwa anaweza kuzimia

Dalili za malaria kwa mtoto pia huambatana na

 • Upungufu wa damu
 • Maumivu makali ya kichwa

Kuzuia Malaria
Malaria ni ugonjwa unaweza kuzuilika iwapo hatua sahihi zitachukuliwa ili kuepuka ugonjwa huo.
Njia zifuatazo zinaweza kutumika ili kuzuia ugonjwa wa malaria usitokee.
1. Kutumia chandarua chenye dawa, hii ni njia sahihi na ya uhakika ya kujikinga na ugonjwa wa malaria. Ni njia sahihi kwani mbu hushindwa kukufikia.
2. Kutumia dawa za kuua wadudu, pia matumizi ya dawa mbalimbali za kuulia wadudu nyumbani kama vile rungu, risasi na nyinginezo zinaweza kutumika katika kuwatokomeza mbu nyumbani. Hata hivyo tahadhari ichukuliwe kwani dawa hizo zinaweza kuleta madhara zikitumika vibaya. Miongoni mwa tahadhari hizo ni kuweka mbali na watoto, kuondoka chumbani kwa dakika kadhaa baada ya kupulizia dawa, usivute harufu ya dawa kwa makusudi na usipulize dawa mahali penye chanzo cha moto kwani inaweza kusababisha mripuko na kuleta matatizo makubwa,
3. Kufyeka nyasi ndefu zinazozunguka mazingira ya nyumbani. Nyasi ndefu hutunza maskani ya mbu hivyo kukata nyasi au vichaka karibu na nyumabani ni njia mojawapo ya kuweza kuwatokomeza mbu.
4. Kufukia mabwawa na madimbwi ya maji na maji yaliyotuama. Kufukia mabwawa na maji yaliyosimama ni njia nzuri ya kuzuia mazalia ya mbu. Ni kawaida ya mbu kuzaliana katika maji yaliyosimama na vibwawa vidogovidogo.

Tiba ya malaria
Ugonjwa wa malaria unatibika kwa urahisi iwapo hatua za haraka za kimatibabu zikifanyika. Kuna dawa nyingi sana zinazotumika kutibu ugonjwa wa malaria. Miongoni mwa dawa hizo ni ALU, Quinine, Malaffin na nyinginezo.
TAHADHARI: Usitumie dawa kujitibu malaria bila ya kupata ushauri/ maelekezo kutoka kwa Daktari. Kwani dawa sahihi itakayokusaidia kutibu malaria huzingatia vigezo vifuatavyo.
i. Aina ya malaria
ii. Kama uliwahi kutumia dawa za kuzuia malaria au hapana
iii. Wapi ulipata malaria(mahali)
iv. Je, mgonjwa ni mjamzito au hapana
v. Hali ya homa
Hivyo kuchukua dawa na kumeza kwa lengo la kujitibu malaria bila ya maelezo ya daktari ni hatari kwa afya yako kwani inaweza kusababisha matatizo zaidi.

Matatizo yanayosababishwa na malaria
Ugonjwa wa malaria unaweza ukauletea mwili matatizo mbalimbali ndani ya muda mfupi kama hatua za kimatibabu hazitachukuliwa. Waathirika wakubwa katika ugonjwa huu wa malaria ni mama mjamzito, watoto wadogo na wazee ingawa hata vijana unawaathiri kwa kiasi chake. Yafuatayo ni matatizo au athari zitokanazo na ugonjwa wa malaria.

 • Kifo. Mara nyingi malaria husababisha kifo. Ugonjwa wa malaria huweza kusababisha kifo kama haukutibika mapema. Ripoti iliyotolewa na shirika la afya duniani mwaka 2015 inaonyesha kuwa ugonjwa wa malaria ulisababisha vifo 584,000 duniani mnamo mwaka 2013
 • Upungufu wa damu mwilini. Ugonjwa wa malaria pia huweza kusababisha upungufu wa damu mwilini. Hali hii hutokea pale seli za damu nyekundu zinaposhambuliwa na kushindwa kuchukua/kubeba oksijeni ya kutosha.
 • Matatizo ya ini
 • Matatizo ya figo
 • Matatizo ya malaria kwa mama mjamzito ni kuharibika kwa ujauzito

*Mtoto kuzaliwa kabla ya wakati (njiti)
*Kifo kwa mama na mtoto
*Mtoto kuzaliwa na uzito pungufu
*Mtoto kushindwa kukua akiwa tumboni
Pia ugonjwa wamalaria husababisha kuyumba kwa uchumi wa nchi kwani pesa nyingi hutumika katika mipango mbalimbali ya kiukomesha malaria. Pesa hizi zingeweza kutumika katika nyanja nyingine za kiuchumi na kuliongezea taifa mapato.

Muda muafaka wa kupata vipimo vya malaria
Inashauriwa na ni vizuri kwa ajili ya usalama wa afya yako kupima malaria mara kwa mara kama unaishi katika maeneo yenye ugonjwa wa malaria. Sababu ya kupima ni kwamba wakati mwingine vijidudu wanaosababisha malaria huingia katika mwili bila kuonyesha ishara yoyote ya ugonjwa, kupima kutakusaidia kutambua hilo na kuchukua hatua sahihi ili kuepuka ugonjwa hapo baadae.
Pia endapo utaona dalili zozote za malaria unatakiwa kumuona daktari haraka iwezekanavyo kwa ajili ya vipimo. Vipimo vya malaria huchukua siku moja tu na lazima upate majibu ndani ya siku hiyohiyo. Kiasi kidogo cha damu huchukuliwa ili kupima kama kuna uwepo wa vijidudu vya malaria.
Ikigundulika kuwa una vijidudu vinavyosababisha malaria fanya mambo yafuatayio
* Sikiliza vizuri ushauri kutoka kwa daktari
* Kama umepatiwa dawa tafadhali maliza dozi. Watu wengi wanapopatiwa dawa hutumia na baada ya kuona hali ya afya imerejea huacha kutumia dawa. Ni hatari kubwa sana ya kutomaliza dozi kwani ikiwa haujamaliza dozi na baadae ukaumwa tena malaria dawa za mwanzo zinaweza zisikusaidie tena, kwa nini? Sababu ni kwamba ikiwa umeacha kumaliza dozi na baadhi ya vijidudu ambavyo havijafa bali vimelewa tu na dawa hurudi katika hali yao ya kawaida na hujenga mazoea na dawa uliyotumia hivyo hata ukatumia tenadawa hiyo baadae haitowaathiri.
* Pia angalia ni kosa gani ulifanya mwanzo hadi ukaambukizwa malaria kama ulikuwa haulali katika chandarua chenye dawa anza sasa kutumia chandarua.
Hali halisi ya malaria
Kutokana na juhudi kubwa za kutokomeza ugonjwa wa malaria zinazofanywa na serikali, mashirika na taasisi mbalimbali duniani, ugonjwa wa malaria hupungua siku hadi siku.Kutokomeza malaria si jukumu la serikali tu au mashirika bali kila mmoja anatakiwa kuchukua hatua sahihi za kutokomeza ugonjwa huu wa malaria kwa manufaa ya mtu binafsi,familia na taifa kiujumla.

Tags:
About Author: Abdallah Hemedi