Kipindupindu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria. Bakteria hushambulia mfumo wa chakula na kusababisha kuhara na kutapika. Kwa kawaida kinyesi cha mgonjwa huwa mithili ya maji meupe. Takwimu kutoka shirika la afya duniani (WHO) zinaonyesha kuwa takribani watu 21,000 hadi 143,000 kila mwaka hufariki kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.
Kuenea kwa kipindupindu: Ugonjwa wa kipindupindu huenezwa na nzi. Ni ugonjwa unaoenea kwa kasi sana. Ugonjwa wa kipindupindu huathiri watu wengi ndani ya muda mfupi sana.

Historia ya ugonjwa wa kipindupindu
Ugonjwa wa kipindupindu ulikuwepo katika bara la Amerika tangu miaka ya 1800 (karne mbili zilizopita) na kuendelea. Kipindupindu hutokea sana sehemu zilizo na hali duni za usafi, zenye mrundikano wa watu wengi, sehemu zenye vita na njaa. Maeneo ambayo ugonjwa huu hutokea mara kwa mara ni pamoja na Africa, Asia kusini na baadhi ya sehemu za Amerika.

Dalili za kipindupindu
Dalili za kipindupindu huweza kuonekana baada ya masaa machache au hadi siku 5 tangu mtu alipoambukizwa, mara nyingi dalili za kipindupindu hazionekani kwa kiasi kikubwa lakini bado mgonjwa anaweza kumuambukiza mtu mwingine.

 1. Kuharisha mara kwa mara. Hali ya kutapika husababishwa na vijidudu kuvamia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
 2. Kutapika
 3. Mwili kukosa nguvu, kutokana na kupoteza kwa kiasi kikubwa cha maji mwilini
 4. Ngozi kusinyaa hali hii husababishwa na upungufu mkubwa wa maji mwilini. Mazingira haya hupelekea kupata kipindupindu.

Kuzuia kipindupindu
Ili kuzuia ugonjwa huu tunatakiwa kufanya yafuatayo.
1. Kudumisha usafi wa mwili na mazingira.
(a) Nawa mikono kwa sabuni kabla na baada ya kutoka chooni.
(b) Nawa mikono kabla na baada ya kula, hapa wengi wanajisahau katika kula matunda. Tabia ya kununua tunda na papo hapo kuanza kula bila ya kuliosha ni hatari sana kwani unaweza ukapata maambukizi ya kipindupindu kwa urahisi.
(c) Vyoo visafishwe kila siku na vifunikwe. Vyoo visafishwe kwa sabuni au dawa maalumu za chooni.
2.Kuchemsha maji kabla ya kunywa. Kuchemsha maji husaidia kuua vijidudu vilivyopo.
3.Kuepuka kula vyakula vilivyo katika mazingira machafu. Matunda lazima yaoshwe kabla ya kuliwa, pia vyakula vilivyo vichafu vitupwe au kufukiwa ili kuzuia mazalia ya nzi.
4.Kuondoa mazalia ya nzi. Maji machafu yamwagwe, masalia ya vyakula yaondolewe haraka na kutupwa mahali sahihi ili kuzuia mazalia ya nzi.
5.Kuepuka kujisaidia ovyo. Watu wasijisaidie ovyo bali wajisaidie mahali sahihi (chooni). Imekuwa ni kawaida watu kujisaidia vichakani hasa vijijni. Hii ni hatari sana kwani husababisha kuenea kwa haraka kwa ugonjwa huu.
6.Chanjo ya mdomo ya kipindupindu ni njia nyingine ya kuweza kuzuia ugonjwa huu.
Maji yatunzwe kwenye vyombo safi na yafunikwe, Kufanya hivi kutasaidia kuzuia nzi wasiyafikie maji kiurahisi.

Ushauri: Tumia maji safi na salama (yaliyochemshwa na kuchujwa, ya kwenye chupa viwandani na yaliyowekewa dawa waterguard katika kufanya mambo yafuatayo.

 • Kunywa
 • Kuandaa chakula na vinywaji
 • Kutengeneza barafu
 • Kusafisha meno
 • Kuosha uso wako na mikono
 • Kuosha vyombo vya kutunzia maji na vyombo vya kupikia
 • Kuosha matunda na mboga kama vile mchicha

Epuka kula vyakula hivi ili ubaki salama

 • Matunda yasiyomenywa
 • Maziwa yasiyochemshwa
 • Nyama iliyopikwa na haikuiva vizuri
 • Samaki wanaopatikana katika kanda za kitropiki pia huweza kuambukiza kwa hiyo kuwa na tahadhari juu ya hayo.

Kumhudumia mgonjwa wa kipindupindu
Ni jukumu la ndugu wa karibu kumhudumia mgonjwa wa kipindupindu, lakini inahitajika tahadhari ya kutosha ili kuweza kuepuka maambukizi kutoka kwa mgonjwa.
– Usishike majimaji au kugusa kinyesi kwa mikono wazi
– Muhakikishie mgonjwa hali ya juu ya usafi
– Usimpe mgonjwa maji mengi ya kawaida bali tumia Maji yenye mchanganyiko wa chumvi na sukari
– Muwaishe mgonjwa hospitali au katika kituo cha afya kilicho karibu nawe
– Usimfiche mgonjwa ndani. Inapendekezwa mara nyingi mgonjwa kukaa sehemu maalumu ambayo haina muingiliano mkubwa wa watu ili kuzuia maambukizi

Tiba ya kipindupindu
ORS (oral rehydration salt) hutumika kutibu kipindupindu, kwa kurudisha kiasi cha maji mwilini.

Athari za kipindupindu
Ugonjwa wa kipindupindu una athari nyingi sana kwa watu na Taifa kiujumla.
– Kifo: Mara nyingi ugonjwa huu unapotokea husababisha vifo vya watu wengi. Husababisha huzuni kwa ndugu waliobaki na simanzi.
Kudorora kwa uchumi: pia kipindupindu husababisha kudorora kwa uchumi kupitia
i.Nguvu kazi inayopotea kutokana na vifo
ii.Serikali huelekeza fedha nyingi katika kuukabili ugonjwa huu
– Athari za kielimu, pia kipindupindu huleta changamoto kubwa katika sekta ya elimu pindi kinapotokea. Iwapo ugonjwa huu ukitokea shuleni au vyuoni,husababisha shule na vyuo kufungwa na hivyo kuwafanya wanafunzi wakose masomo kwa muda fulani.

Tags:
About Author: Abdallah Hemedi