Katika familia nyingi duniani suala la ugomvi sio kitu cha kushangaza, kwa sababu ni kawaida kwa binadamu wanao kaa pamoja kugombana kutokana na sababu mbalimbali. Hakuna wanao kaa pamoja maisha yao yote pasipo kutofautiana na kugombana.

Hakuna ugomvi usiokua na madhara, lakini madhara yenyewe yanategemea na aina ya ugomvi, mfano madhara ya ugomvi wa watu wanao tupiana maneno hayawezi kulingana na madhara ya ugomvi ambao watu wamepigana. Hivyo hivyo kwa aina nyingine zote za ugomvi.

Lakini hapa nataka kuongelea madhara ya ugomvi wa wanandoa,wazazi au walezi kwenye familia zetu hasa za kiafrika ambapo tabia hii imekithiri na labda ni kwa sababu hatujui madhara yake.

Ni jambo la kawaida sana kukuta wazazi wa familia nyingi za kiafrika wakigombana na kufikia kabisa hatua ya kupigana mbele ya watoto wao bila kujali kitu chochote kile, nyumba inageuka uwanja wa mapambano na watoto ndio wanao jikuta wakiwa waamuzi wa ugomvi huo wa wazazi wao.

Mbali ya kuwa ni aibu kwa wazazi hao mbele ya watoto wao lakini pia ni jambo linalowapa mateso makali watoto wanaoishi na wazazi wenye tabia hizo. Lakini jambo baya kwa watoto hawa ni madhara wanayo yapata kisaikolojia hali inayopelekea kuwa watu wenye tabia tofauti ambazo ni matokeo ya ugomvi wa wazazi wao waliokuwa wakihishuhudia katika utoto wao.

Sasa je, ni nini madhara ya wazazi kugombana mbele ya watoto wao?

Wanasaikolojia wanalizungumzia suala hili kama ni moja ya makosa makubwa ambayo yanapaswa yakemewe kwa nguvu sana maana madhara yake ni mabaya kwa jamii nzima na sio tu kwa wanafamilia hao. Ikumbukwe kuwa mjenzi wa kwanza wa tabia ya mtoto ni wazazi, hivyo basi kama wazazi hawa ambao ndio walezi wakuu watashindwa kutimiza wajibu wao ni wazi kabisa jamii nzima itapata madhara kwa uzembe huo. Inaelezwa kuwa kitendo cha wazazi kugombana mbele ya watoto wao kina madhara ambayo huathiri mfumo mzima wa maisha wa watoto wa familia izo hasa wanapokua watu wazima, ambapo ina aminika kwamba watoto hao huwa na tabia ambazo huenda ikawa ni za kushangaza au hata kukera watu wengine.

Miongoni mwa tabia wanazokuwa nazo watoto ambao wamekulia katika familia zenye ugomvi ni kama zifuatazo:

Ukatili
Ni jambo la kawaida sana kwa watoto walio kulia katika familia za aina hii kua na roho za kikatili. Hawaoni kama ni jambo la ajabu kumfanyia mtu mwingine vitendo vya ukatili, huwa hawana huruma kwa kitu chochote kile, hii ni kutokana na matukio ya ukatili walio wahi kuyashuhudia tangu wakiwa watoto. Mfano, mtu ambae katika utoto wake ameshuhudia ugomvi uliopelekea mtu mmoja kumuua mwenzake ni rahisi sana kwa mtoto huyo kuja kufanya tukio kama hilo la mauaji.

Ubishi
Kwa haraka haraka linawezekana lisionekane kama ni tatizo lakini pia sio jambo zuri kwa mwanadamu kama likizidi, inaelezwa kuwa watoto waliokulia katika familia zenye migogoro ya mara kwa mara huwa ni wabishi na huwa wanaamini katika kile wanachokiamini hata kama wengine watakiona ni cha utofauti, mara nyingi husimamia Imani yao hata kama hawana mifano hai ya kukitetea icho anachokiamini.

Kutokujali
Hakuna tatizo kubwa kwao, suala lolote lile kwao ni la kawaida hawashtuki na chochote kile, tabia hii inawafanya wawe ni watu wenye kupuuza jambo lolote lile hata kama litakua kubwa kiasi gani. Matukio walio shuhudia utotoni yanawafanya wawe watu wa aina hii.

Ukorofi
Hii ni tabia ambayo watoto hawa ni lazima wawe nayo ni tabia walioiishi tangu utoto wao, wameshuhudia ugomvi na ukorofi kutoka kwa wazazi wao, wakiamka ugomvi wakilala usiku ugomvi, hivyo nao wanajengeka katika tabia iyo ya ukorofi ni mara chache sana kuwakuta watoto waliotoka kwenye familia hizi kuwa wastaarabu.

Lakini mbali na kuwa na tabia hizo, wanasaikolojia pia wanasema watoto walio kulia kwenye familia hizo huwa na uwezo sana wa kukabiliana na matatizo katika maisha yao na pia ni wazuri katika kuamua jambo lolote lile hata kama ni gumu kiasi gani.

Hivyo kama wewe ni mzazi na una tabia ya kugombana mbele ya watoto wako ni vyema ukabadilika maana madhara yake kwa watoto ni makubwa, jaribuni kuficha tofauti zenu mbele ya watoto wenu na badala yake muwaonyeshe na kuwafundisha kuishi kwa upendo ili waje kuwa wazazi bora na wenye tabia zuri kwenye familia zao.

Makala hii imeandaliwa na Geofrey Shao kwa msaada wa Neema Mwacha, mwanasaikolojia na mtoa mshauri nasaha.

Tags:
About Author: Geofrey Shao