Ugonjwa ni hali ya kimwili mbali na jeraha ambayo huingiliana na utendaji kazi wa kawaida wa mfumo wa mwili. Mwili wa kiumbe hai (mfano: binadamu) una mifumo mbalimbali ambayo inauwezesha mwili kufanya kazi kiufanisi. Iwapo itatokea hali itakayoyumbisha ufanyaji kazi wa mifumo hiyo, hali hiyo hujulikana kama ugonjwa. Kuna magonjwa mbalimbali Duniani na kila siku yanazidi kuongezeka mapya. Leo ningependa tuangalie sababu kuu zinazosababisha ugonjwa kwa binadamu. Kila ugonjwa una sababu yake na kwa kufahamu sababu ndipo tiba sahihi hupatikana. Zifuatazo ni sababu kuu za magonjwa

i. Vijidudu vya magonjwa
Vijidudu mbalimbali kama vile virusi, bakteria, plasmodiam na fangasi husababisha magonjwa mbalimbali. Magonjwa yanayosababishwa na vijidudu mara nyingi huwa ni ya kuambukiza, yaani huweza kuenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa wengine.
Vijidudu hivi huingia katika mwili wa binadamu kupitia ngozi, mdomo na sehemu nyingine zilizo wazi.
Magonjwa yanayosababishwa na virusi ni Ukimwi, mafua, surua, tetekuwang, kichaa cha mbwa na mengineyo.
Magonjwa yanayosababishwa na bakteria ni Kipindupindu, taifodi, Kaswende, Kichocho, Kisonono na mengineyo.
Magonjwa yanayosababishwa na fangasi ni Ukungu sehemu za siri, Yabisi, na mengineyo.
Magonjwa yanayosababishwa na plasmodiam ni Malaria.

Tahadhari: Watu wengi huchanganya kati ya vijidudu vinavyosababisha Ugonjwa na wadudu/wanyama wanaousambaza. Wadudu kama mbu, nzi, mbung’o na panya hawasababishi magonjwa bali wanaeneza magonjwa, na wengine wanatunza vijidudu vya magonjwa.

ii. Utapiamlo
Hii ni hali ya kula kupita kiasi, kula chini ya kiwango kinachohitajika au kukosa aina Fulani ya virutubisho katika mwili wa binadamu. Kwa ufupi neno utapiamlo lina maana Lishe duni (utaratibu mbaya wa mlo). Kula sana au kula chini ya kiwango au kukosa aina Fulani za virutubisho mwilini husababisha Magonjwa. Magonjwa yanayosababishwa na matatizo ya lishe ndio hujulikana kama Utapiamlo.
Kuna magonjwa mbalimbali yanayosababishwa kutokana na matatizo ya chakula yakiwemo Kiribatumbo, Marasmas, Matege, Rovu, Unene usio wa kawaida, Kutoona vizuri usiku, na mengine mengi. Magonjwa ya aina hii hayaambukizi, yaani hayawezi kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mara nyingi magonjwa haya huwapata watoto hasa walio katika umri chini ya miaka 5, na yapo kwa wingi katika bara la Afrika na mashariki ya Kati, kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi katika maeneo hayo.

iii. Sababu za kiurithi
Sababu nyingine ya Magonjwa ni urithi, yaani mzazi humrithisha mtoto wake ugonjwa aliokuwa nao. Mfano mzuri wa magonjwa ya kurithi ni Seli mundu, huu ni ugonjwa ambao seli za damu nyekundu hupoteza umbo lake la duara na kuwa na umbo la upinde, seli zenye umbo la upinde hufa haraka na hivyo husababisha upungufu wa damu mwilini na hata kifo. Ugonjwa mwingine wa kurithi ni Haemofilia, Huu ni ugonjwa wa kutoka kwa damu kusiko kwa kawaida.

iv. Mtindo wa maisha
Wakati mwingine jinsi mtu anvyoishi hupelekea kuugua. Kwa mfano kutofanya mazoezi na kukaa kwa muda mrefu hupelekea magonjwa ya viungo na miguu kujaa maji. Pia kula vyakula vya mafuta kwa wingi na huongeza kasi ya kupata magonjwa ya moyo. Uvutaji wa sigara hupelekea magonjwa ya mapafu.

v. Matatizo ya homoni
Homoni ni kemikali zinazofanya kazi maalumu katika mwili wa binadamu. Homoni huzalishwa na tezi mbalimbali. Upungufu au wingi wa homoni kupita kiasi husababisha magonjwa katika mwili wa binadamu. Kwa mfano Ugonjwa wa Rovu unahusianishwa na upungufu wa homoni ya thairoksin.

Tags:
About Author: Abdallah Hemedi