Mapenzi ni kitu kilichoumbwa kwa ustadi wa juu ili kumfanya mwanadamu apate furaha na faraja ya kweli katika moyo wake na yule anayempenda. Ni ukweli usio na shaka kuwa katika maisha ya binadamu yoyote yule mapenzi ni kitu kinachohitajika sana.

Kila mtu anaweza akayaongelea mapenzi kwa kadri alivyowahi au jinsi anavyoyaishi mapenzi katika wakati husika, kuna watakao yaongelea mapenzi kama ni kitu ambacho hawawezi kuishi bila kuwa nacho hawa ni watu ambao wako kwenye mahusiano na watu sahihi ambao kweli wamependana nao, lakini pia kuna wengine watayaongelea mapenzi kama ni kitu kibaya walichowahi kukutana nacho maishani. Hawa kila mtu kwa sababu zake anaweza kuelezea sababu na ubaya wa mapenzi katika maisha yake, wapo waliosalitiwa na wenza wao, wapo walioachwa bila kutegemea wala kujua sababu za kuachwa na wenza wao. Lakini pia wapo wanao yachukia mapenzi kwa sababu wao ndio waliolazimisha mapenzi kwa watu wasio na mapenzi nao, ukweli, lakini zaidi ya yote hawana hisia nao.

Hiki ndicho ninachotaka kukizungumzia, tafiti nyingi zilizowahi kufanywa na watafiti wengi duniani zinaonyesha kuwa wavulana na wasichana wengi ambao walilazimisha mapenzi kwa wenza wao wanaishia kutendwa na kuumizwa na wapenzi wao hao.

Mara nyingi wavulana au wasichana hupenda kudumu na wapenzi ambao wamewachagua wenyewe kuliko wale ambao wamelazimisha kuwa nao kwa sababu mbalimbali. Utamu wa maisha katika mahusiano utauona kama tu utakuwa na mtu ambaye umemridhia naye amekuridhia siyo mtu ambae labda wewe unampenda alafu yeye hakupendi au yeye anakupenda alafu wewe humpendi.
Inawezekana kuna watu wengi walioanzisha uhusiano wa kulazimisha wameshindwa kudumu katika mahusiano hayo kwa sababu mbalimbali kama ifuatavyo:

1. Kukosekana kwa uaminifu katika mahusiano hayo
Utafiti mwingi unaeleza kuwa mahusiano ya kulazimisha huwa yanakosa uaminifu hali inayotokana na wawili hawa kutoridhiana, hali hii hupelekea usaliti ambao ndo ukosekanaji wa uaminifu na hivyo kusababisha wawili hawa kuachana.

2. Hisia /Mapenzi
Hisia ni kila kitu katika mahusiano yote duniani, hakuna uhusiano unaoweza kudumu pasipo kuwa na hisia kwa wawili hawa wanaopendana, kutokana na ukweli huo watu wengi wanaojiingiza katika mapenzi ya kulazimisha wanajikuta wakiumizwa na mwisho uhusiano kuvunjika kwa sababu ya kukosekana kwa hisia kati yao, hii ni kutokana na mmoja kutokumridhia mwenzie kutoka katika mtima wa moyo wake.

3. Kutokujali
Hii pia ni moja kati ya sababu zinazopelekea mahusiano ya kulazimisha kuvunjika, hakuna asiyependa kupata au kufanyiwa chochote na mpenzi wake kama sehemu ya care katika mahusiano, kujali pia ni sehemu muhimu ya maisha ya mahusiano. Uhusiano wowote wa kulazimisha huwa unakosa kiungo hiki muhimu hii ni kwasababu kama uko na mtu ambaye hajakuridhia hawezi kujitoa wala kujali chochote kuhusu wewe na kutokana na hali hii ni vigumu sana kwa mahusiano ya namna hii kudumu.
Hizo ndizo sababu kuu zinazosababisha mahusiano ya kulazimisha kuwa msiba wenye maumivu makali sana kwa baadhi ya watu.
Ushauri kwa msomaji mpenzi wa makala hii; Ili uweze kufanikiwa katika ndoto zako katika ulimwengu wa mahusiano ni vyema kuanzisha uhusiano na mtu ambaye mnaridhiana kutoka katika vilindi kabisa vya mioyo yenu. Siku zote unapoishi na ambaye anakuridhia kutoka moyoni anaweza kufanya lolote kwa ajili yako ili asikupoteze na hapo ndipo utakapo hisi kuwa dunia yote ipo chini ya miguu yako.

That is the power of love!

Tags:
About Author: Geofrey Shao