Ilikua ni majira ya jioni tulivu, nikiwa naambaa ambaa pembezoni mwa bahari ya Hindi, upepo mwanana ukivuma taratiiiibu….. Ni huko mkoani Lindi kusini mwa Tanzania, ndipo nilipoamua kukaa chini ya mti wa mkorosho penye kivuli mwanana nikishuhudia mawimbi ya maji ya bahari kwa madaha yakijongea kuja ufukweni. Ama kwa hakika bahari ina raha yake jamani na ningekua na uwezo nigechimba bahari kwetu Mbeya au ningeihamisha Mbeya kuipeleka karibu karibu na Zanzibar.

Baada ya kitambo kidogo niliikumbuka ile siku, siku niliyokwenda kwenye ofisi za mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa fulani, nilipokutana na mama yule mzee aliyebakisha miaka michache sana kustaafu. Mama yule alipogundua katika mazungumzo yetu kwamba nimesomea masuala ya mifugo, alijisononekea sana.

Alisema ee mwanangu, tazama mimi mama yako, umri umenitupa mkono sasa, nimeajiriwa hapa miaka yote, bado ningali mtu wa kawaida mno.
Nalitamani kujihusisha na mambo ya kilimo nijiajiri lakini nagundua nimeshachelewa sana. NAONA BORA NIMALIZIE TU nistaafu zangu mambo yaishe.

Aliendelea mama yule kwa huzuni kubwa, anatamani sana angekua kama Mimi, angekua na umri kama Wangu na taaluma kama Yangu. Asingethubutu kuajiriwa kwa ajili ya “vi-laki tatu”, akasema angejiajiri mwenyewe na angefika mbali sana. Alisisitiza kwamba kilimo kinalipa Sana, alinisihi nikafuge chochote ninachopenda kitanilipa. Ilikua ni kauli yake ya mwisho mama yule wa TRA.
Wakati naondoka katika zile ofisi nilikua nikitafakari na kujiuliza sana, hivi huyu mama yaani anakitamani kilimo wakati yuko TRA ? TRA hii hii ambayo kila mtu anaitamani ? Amerogwa na nani huyu ?

Nilimfikiria kijana wa leo, kijana aliyemaliza chuo, amesomea kilimo, anavyoisubiri serikali ifungue Ajira, anavyohangaika mitandaoni kutafuta NAFASI ZA KAZI, anayefikiria kwamba kusoma kilimo alikosea ni bora angesomaga ualimu au angeendaga UPOLISI, mfano wa kwanza wa kijana ninayemfikiria nikawa mimi mwenyewe.

Nikagundua kwamba wakati mimi natamani kuwa kama Fulani, yeye anatamani angekua japo nusu yangu. Nikamkumbuka mtu mwenye Masufuria, sahani, jiko, unga na mboga anayeenda kupikia kwenye jiko la jirani yake na akishaivisha wenyeji wanampimia chakula.

Huo ndio ulikua mwisho wa kumkumbuka yule mama mtu mzima.

Niliamka pale chini ya mkorosho, ufukweni mwa LINDI nilipokua nimekaa, nikabeba begi langu na kwenda zangu huku nikijisemea kimoyomoyo “LABDA NAMIMI NITAJIFUNZA NIKIZEEKA”.

Tags:
About Author: Emmanuel Julius