Kitendo cha kuchukua hatua na kuanza kufanya jambo ni moja kati ya uamuzi sahihi katika maisha ya mtu yoyote yule duniani. Watu wengi tumekwama hapa, tunahitaji uhakika kwanza. Je, hili wazo ni la kweli na litaleta matokeo sahihi? Kutokana na kuwa na imani ndogo na kutokujiamini kwetu, akili inatoa jibu la kwamba hilo wazo au huo mpango hautafanikiwa na haya majibu ni sahihi kwa akili yako kutokana na ukweli akili zetu tumezijaza woga na hofu.

Ndoto nyingi, mawazo mengi ya biashara yamefia hapa, au yameishia katika hatua hii ya kufanya uamuzi. Akili inatoa jibu kulingana na aina ya taarifa ulizozijaza katika kichwa chako, kama umejaza woga na kutojiamini, basi majibu yatakayotoka ni yanayofanana na taarifa hizo za woga na kadhalika. Pia kukosa kujiamini kumekwamisha mafanikio ya watu wengi na kwa kutokujua kwamba kushindwa kuchukua uamuzi ndio kuna wakwamisha kimaisha.

Watu wengi wanaishi maisha ambayo hawaja rizika nayo au kupendezwa nayo kwa namna moja ama nyingine. Lakini wengi wao wanakosa ujasiri wa kutaka kupambana na hali wasizozipenda ili kuondokana nazo. wengi wameishia katika kulalamika na mwisho wa siku kukata tamaa kabisa.

Wengi wanaacha mambo yaende kama yalivyo bila hata kuonesha juhudi za kuyarudisha au kuyatengeneza kwa jinsi wanayoitaka. Kila aina ya maisha inatengenezwa na mtu mwenyewe, aina ya maisha unayoyaishi sasa umeitengeneza wewe mwenyewe na maisha yajayo una yatengeneza wewe mwenyewe sasa.

Uhalisia wa maisha yetu huanzia kwenye mifumo yetu ya fahamu hasa akili, kwa jinsi unavyoiongoza akili yako ndivyo itakavyokufikisha mahali unapopataka. Hii ni kutokana na akili ndio kitu pekee kinachotutenganisha au kututofautisha binadamu na mnyama, akili yako ni kitu chenye nguvu ya mabadiliko na maendeleo kwako.

Kukosa kujiamini kunajitokeza katika aina mbalimbali kwa mfano kusita kufanya jambo fulani ambalo moyo na akili vinaamini ni sahihi kwako na kama utalifanikisha litaweza kubadili maisha yako na kukutoa sehemu moja kwenda nyingine.

Lakini kila siku ukiishia kuwaza tu na hakuna hatua yoyote unayoichukua kuelekea kukamilisha huo mpango wako, kila siku unakosa ule msukumo wa kufanya hilo jambo, hiyo ni dalili pia ya kukosa kujiamini. Watu walio katika hali kama hii wanakuwa na mawazo na michango mizuri sana na inavutia kusikiliza.

Inaweza kua ni mawazo ya biashara yaliyo na tija, lakini kwanini hawayafanyii kazi kwanini hawazitumii fursa wanazoziona? Jibu ni kwamba hawajiamini, hofu ipo ndani yao ambayo ata wao wanaweza kujikuta hawaitambui ila ipo na inawarudisha nyuma kwenye kila kitu kipya wanachotaka kukifanya.

Kujiamini kunatengeneza kitu kimoja muhimu sana ndani ya mtu; UTEKELEZAJI.

Watu wengi siyo watekelezaji wa kile wanachokipanga au kukisema hii ni aina nyingine ya kukosa kujiamini.

Watu ambao sio watekelezaji wa ahadi zao na mipango yao, mara nyingi inakuwa vigumu kwao kufanikiwa. Kushindwa kutekeleza jambo ulilolipanga mwenyewe ni tabia ya uzembe na uvivu uliotukuka. Mafanikio ni matokeo katika kuamua.

Kuna tatizo katika utekelezaji watu wengi wanafanya vitu kwa ujumla tu bila kuingia kwa kina lakini pia kufanya jambo bila ya kujituma, kukosekana kwa udadisi ni dalili ya kushindwa, kuna tatizo la kutokupenda kujifunza vitu vipya watu hawapendi kusumbua akili zao hata kidogo.

Jinsi unavyo itumia akili yako katika kujifunza kitu kipya ndivyo unavyo piga hatua mbele zaidi kuyaelekea mafanikio yako, mafanikio yapo katika kujituma, kujifunza, kuamua na kufanya. Ni vyema mtu kujaribu jambo lolote la mafanikio katika maisha yako bila kujali kushindwa au kuchekwa na watu eti kwa sababu umejaribu umeshindwa. Pambana kila wakati kwa ajili ya ndoto zako, ndoto zako ndio ziwe dira ya maisha yako.

Watu wengi mashuhuri tunaowasikia hivi sasa walipambana katika walicho kiamini na hakuna aliye fanikiwa bila kushindwa njiani, kushindwa ni ishara ya inayoonyesha kuwa unakaribia kufika ulipo pataka ila tu kama utaamua kunyanyuka na kuendelea kupambana.

Hata mwandishi wa makala hii pia amepambana katika kufikia lengo lake hii la uandishi, hakuna kitu kinachokuja kwa urahisi ni lazima ukitafute kwa nguvu zote bila ya kukata tamaa, lakini ili kuyaweza hayo yote ni lazima kwanza ukubali kuamua, kujaribu na mwisho wa siku kufanya kabisa kile ulichokitaka kwa maendeleo yako mwenyewe.

Tags:
About Author: Geofrey Shao