Katika jamii nyingi za kiafrika swala la kutopatikana aina fulani ya watoto huwa ni sababu inayosababisha ndoa nyingi sana kuingia katika mafarakano na hata nyingine kufikia hatua ya kuvunjika eti kisa mama anazaa watoto wa kike tu au anazaa watoto wa kiume tu.

Uelewa mdogo wa watu wengi huwa ndo chanzo cha matatizo katika ndoa nyingi bila ya kujua kuwa ni swala lao wote wawili na wala siyo la mtu mmoja hasa mama ambae ndio anayeonekana mara nyingi kuwa yeye ndio mwenye matatizo.

Wataalamu wa mambo ya uzazi wanaelezea bayana kuwa si mama ambae ndie anaamua kubeba mimba ya mtoto wa kiume au ya mtoto wa kike.

Wakielezea katika vitabu mbalimbali wataalamu wengi husema kuwa mwanamke huzalisha mbegu za aina moja zinazotambulika kama “XX” na mbegu hizo huendeleza ukike, wakati nwanaume huzalisha mbegu za aina mbili ambazo ni ‘X’ (kike) na ‘Y’ (kiume).

Tafiti zinaelezea na kuthibitisha kuwa mbegu yoyote ya mwanamke ( ‘X’) ikichavushwa na mbegu ‘X’ ya mwanaume hutengeza muunganiko wa ‘XX’ ambao matokeo yake ni kutungwa kwa mimba ya mtoto wa kike, lakini ikitokea mbegu ‘X’ ya mwanamke ikakutana na mbegu ‘Y’ ya mwanaume tokeo la muunganiko huwa ‘XY’ na hivyo ni kutungwa kwa mimba ya mtoto wa kiume.

Sasa je ni nini chanzo cha baadhi ya familia kuwa na watoto wengi wa jinsia moja? Hili ni swala linalowaumiza vichwa watu wengi na hasa waanga wa tatizo hili.

Jibu sahihi la swali hilo ni kwamba daima mbegu ‘X’ na mbegu ‘Y’ zinauwezo tofauti na pia zinatofautiana katika swala zima la uhai mara tu zinapotokea kwa mwanaume na kuingia kwa mwanamke tayari kwa urutubishwaji.

Inaelezwa kwamba sifa kuu ya mbegu ‘X’ ni uimara wake ukilinganisha na mbegu ‘Y’ ambayo siyo imara na hufa mapema, lakini pia mbegu ‘X’ inaelezwa kuwa ina sifa ya kuwa na mwendokasi mdogo wakati mbegu ‘Y’ huwa na mwendokasi sana.

Hivyo kutokuwa imara na kuwa na mwendokasi mkubwa husababisha mbegu hii ya ‘Y’ kufa kama haitakutana na yai katika mwili wa mwanamke na hapa ndipo mbegu ‘X’ inapopata nafasi kwa sababu inauwezo wa kuishi muda mrefu na hivyo huwa na uwezo wa kusubiri mpaka yai litakapokuwa tayari na hivyo kurutubishwa na mbegu ‘X’ ya mwanamke na hivyo kutungwa kwa mimba ya mtoto wa kike.

Lakini baadhi ya wataalamu wa mambo ya uzazi wanaelezea kuwa bado kuna uwezekano wa wanandoa kuchagua jinsia ya watoto wanaowataka katika familia zao.

Inaelezwa kwamba kuna njia kuu mbili ambazo zinawawezesha wanandoa na wote wanaotaka watoto kuchagua jinsia ya watoto wanaowataka. Na njia hizo ni kama ifuatavyo:

1. Njia ya upandikizaji
Inaelezwa kuwa njia za upandikizwaji wa mbegu ndio njia ya uhakika zaidi katika swala la uchaguzi wa jinsia ya mtoto, kwa sababu ni njia inayotumia matumizi ya maabara lakini changamoto kubwa ya njia hii ni gharama kubwa, kitu kinachowafanya watu wengi kushindwa kumudu gharama hizo.

2. Njia ya kalenda
Hii ni njia rahisi na isiyo na gharama kwasababu haihusishi matumizi ya maabara, ila njia hii inahitaji wahusika kuwa makini zaidi katika kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa sababu uzembe wowote utaleta matokeo tofauti.

Jinsi ya kufuatilia njia ya kalenda
Kubwa zaidi katika ufuatiliaji wa njia hii ni afya njema kwa wazazi na muda sahihi wa kushiriki tendo la ndoa.

Kutokana na sifa na tabia ya mbegu zote mbili kama nilivyozielezea uko juu wanandoa wanapaswa kuzingatia mzunguko wa hedhi wa mwanamke ili kufanikisha upatikanaji wa mtoto wa kiume au wa kike.

Jambo la msingi hapa ni lazima wanandoa watambue aina ya mzunguko wa mwanamke husika ni wa aina gani, kwa kawaida kuna mzunguko wa siku 28 ambao katika siku ya 14 yai hutoka , kuna mzunguko wa siku 21 ambao ni mzunguko mfupi na siku ya 10 yai hutoka na pia kuna mzunguko wa siku 36 ambao katika siku ya 18 yai hutoka huu ni mzunguko mrefu zaidi.

Kila katikati ya mzunguko yai hutoka, pamoja na kujua hilo la mzunguko bado tabia za mbegu ‘Y’ ambayo husafiri haraka na mbegu ‘X’ ambayo husafiri taratibu pia zinatakiwa zijulikane maana hilo ndilo husaidia katika kufanikisha swala la uchaguzi wa jinsia ya mtoto.

Kwa kufahamu tabia hizo kumbe wazazi sasa wataweza kuamua mtoto wamtakae kwa kuzingatia uharaka wa mbegu na utokaji wa yai katika mwili wa mwanamke.

Mfano wanandoa wakifanya tendo la ndoa siku moja kabla ya yai kutoka basi mtoto atakaepatikana hapo atakuwa wa kiume kwa sababu mbegu ‘Y’ ambayo inatoka kwa mwanaume ina sifa ya kuwa na mwendokasi hivyo ni lazima yenyewe itakuwa ya kwanza kufika ikiiacha ile mbegu ‘X’ bado iko nyuma kutokana na mwendo wake.

Hivyo hivyo wazazi wakiwa wanataka kupata mtoto wa kike watatakiwa kufanya tendo la ndoa mara nyingi kati ya siku ya 9,10 au 11 kabla ya siku ambayo yai la mama hutoka, hivyo kutokana na mwendokasi na udhaifu wa ‘Y’ itapelekea mbegu hii kuwahi kufika lakini pia ikiwahi kuaribika kutokana na kutokuwepo kwa yai la mwanamke,wakati mbegu ‘X’ inayosafiri taratibu itafika katika muda ambao yai litakuwa limetoka au linakaribia kutoka hivyo kusababisha mimba ya mtoto wa kike kutungwa.

Ila ni lazima itambulike kwamba hizi zote siyo kanuni kwasababu mwili wa mwanadamu hubadilika.

Jambo la kuzingatia ni kutambua aina ya mzunguko na siku na kufanya tendo la ndoa kulingana na tabia za mbegu ‘X’ na ‘Y’. Njia hizi mbili zinaweza kupunguza migogoro katika ndoa nyingi au kuokoa ndoa nyingi kuvunjika.

Maelezo: Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa ndugu Ibrahim Saidi (mwanafunzi wa udaktari chuo cha udaktari Muhimbili).

Tags:
About Author: Geofrey Shao