Chakula ni muhimu sana kwa binadamu na viumbe vyote duniani, lakini jambo la muhimu linalo takiwa katika suala zima la chakula ni jinsi ya uandaaji wa chakula chenyewe. Uchafu wa chakula huweza kusababishwa na vimelea vya maradhi kutoka katika mazingira, wanyama, wadudu au binadamu.

Madhara yatakayojitokeza endapo mlaji atakula chakula ambacho kimeandaliwa vibaya ni kama, vile kuumwa tumbo, kuhara, kuhara damu na hata kuugua kipindupindu na kupoteza kabisa maisha. Madhara haya husababishwa na kutokuzingatiwa kwa kanuni bora za utayarishaji wa chakula salama, majumbani, hotelini, migahawani.

Shirika la afya duniani(WHO) liliwahi kuhainisha mambo yakuzingatia ili uandaaji wa chakula uwe bora na wenye tija kwa walaji wote. Mambo hayo ni kama yafuatayo:

Kuzingatia usafi
Hali ya usafi na tabia binafsi ya muandaaji wa chakula inahusisha mambo yafuatayo; kunawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka msalani, kabla ya kuandaa, au kula chakula baada ya kugusa chakula kibichi mfano; nyama, samaki,na kuku. Pia kugusa takataka au kutoa takataka kwa mikono bila kutumia gloves, kukohoa bila kufunga mdomo,vilevile hata kupiga chafya bila kuziba pua na kitambaa au tishu safi, kugusa sehemu yoyote ya mwili na moja kwa moja kula chakula bila kunawa mikono, na kufanya usafi huku akila na kugusa vyombo vichafu na baadae kula pia.

Ni muhimu kuepuka kushika kwa mikono chakula kilicho tayari kuliwa,isipokuwa kwa kutumia kijiko au chombo kingine kinachofaa. Muandaaji wa chakula anashauriwa kuwa msafi muda wote, kuvaa mavazi safi wakati wa kuandaa na kuepuka kushika sehemu za vyombo ambazo hugusana na mdomo wa mlaji.

Suala lingine muhimu la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa maeneo yote ya kuandalia na kuhifadhi chakula kama vile jokofu na kabati vinatunzwa katika hali ya usafi. Wadudu kama mende na panya hawatakiwi kuwepo katika maeneo ya kutayarishia chakula kwani hubeba vimelea vya maradhi.

Vyombo vya kuandalia chakula kama vile sufuria,sahani, vikombe na vijiko vinapaswa kuwa katika hali ya usafi wakati wote wa maandalizi ya chakula na hata baada ya kutumika.

Kutenganisha chakula kilichopikwa na kibichi
Chakula kilichopikwa kihifadhiwe sehemu safi na kitenganishwe na chakula kibichi kwani chakula kibichi kinakua na uwezekano mkubwa wa kuwa na vimelea vya magonjwa. Wakati wa kupanga chakula katika jokofu, vyakula vibichi viwekwe katika sehemu ya chini ili kuzuia majimaji yake kuchuruzikia na kuingia kwenye vyakula vilivyopikwa.

Chakula kipikwe mpaka kiive vizuri
Ni jambo la msingi sana hili katika uandaaji wa chakula, vyakula kama nyama, mayai na samaki ni muhimu katika kuhakikisha kua vimepikwa hadi vikaiva vizuri, hii sio kwa vyakula ivyo tu bali kwa vyakula vyote chakula kilichoiva vizuri kinakua hakina madhara yoyote kwa mlaji kwa sababu vimelea vyote vya maradhi vilivyopo katika chakula icho vinakua vimekufa. Vyakula vilivyopoa au viporo vinatakiwa kuchemshwa kikamilifu ili kuua vimelea vya magonjwa.

Kuhifadhi chakula kilichopikwa
Baada ya chakula kuiva kinatakiwa kiwekwe kwenye mazingira safi tayari kwa ajili ya kuliwa na wahusika pia inashauriwa chakula kiliwe wakati bado cha moto, endapo chakula kilichopikwa hakita liwa kikiwa bado cha moto basi kinatakiwa kihifadhiwe kwenye chombo kinacho hifadhi joto, ili kuzuia kuzaliana kwa vimelea vya maradhi. Na pia endapo chakula kitabakia baada ya kuliwa basi nacho kinatakiwa kihifadhiwe mahala safi na salama.

Kutumia maji safi
Ni jambo la muhimu kabisa kuhakikisha kuwa maji ya kunywa ni safi na salama. Matunda na mboga mboga za majani vyote vioshwe kwa maji safi na salama. Maji safi na salama ni yale yaliyochemshwa na kuchujwa vizuri, na pia yaliyo hifadhiwa katika chombo safi. Hayo ni mambo muhimu kabisa katika suala la uandaaji wa chakula. Ikumbukwe kwamba chakula bora ndio msingi wa afya bora kwa binadamu wote.

Tags:
About Author: Geofrey Shao