Kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la pili (2010), imeeleza maana ya utandawazi kuwa ni mfumo wa uhusiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali kama biashara, uchumi na siasa.

Mfumo huo umewezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari inayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi na kuchangia ukuaji wa sayansi na teknolojia ambayo imesambaa kwa kasi kubwa na kugusa maisha ya mwanadamu.

Pamoja na dhana halisi ya utandawazi, bado umechangia kuathiri swala zima la malezi na kusababisha watoto na vijana kukosa mwelekeo bora wa maisha kutokana na kulega kwa mawakala wa malezi.

Wakala wa malezi ni Familia, dini, shule, vyombo vya habari pamoja na makundi rika ambao wanajukumu la kuwapatia malezi bora vijana, watoto na jamii nzima kama heshima, nidhamu ili waweze kujiandaa na maisha ya baadae, kushiriki shughuli za uzalishaji bila kupotoka na mambo mabaya yasiyo pendeza katika jamii.

Kutokana na ongezeko la uzalishaji, biashara na kukua kwa miji, kuna sababisha wakala wa malezi kuongezeka kama simu za mkononi, magazeti, majarida mbalimbali na tovuti.

Swala la maadili kwa watoto na vijana ni jambo muhimu ambalo humtambulisha binadamu ndani ya jamii yake. Katika hali ya kawaida, maadili hujitokeza kwenye matendo kwani ndicho kielelezo sahihi cha kupima maadili ya jamii.

Utafiti unaonyesha ya kuwa binadamu wengi wanaamini msingi wa kwanza na mkuu wa maadili unaanzia kwenye familia ambako ndiko mtoto anakoanza kujifunza na kutambua mambo mengi tofauti tofauti, na kuendelea nayo hadi ukomo wa maisha yake hapa duniani.

Maadili yanahitajiwa na watu wote licha ya kuwa kuna nyakati mahitaji kati ya mtu na mtu hutofautiana kwa kuzingatia mitizamo ya kilimo, siasa, jiografia, utamaduni au falsafa na mitizamo ya jamii husika.

Teknolojia inatajwa kuwa ni moja ya sababu inayofanya dhana ya maadili kuwa tofauti na kuongelewa kuwa ni moja ya kichocheo cha kubadili mienendo na maisha ya binadamu bila kujali na kuheshimu misingi ya maadili.

Mabadiliko haya yamejikita sana katika matumizi ya mitandao ya kijamii kama Whatsapp, Instagram na Facebook ambayo vijana wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwasiliana na watu mbalimbali.

Matumizi mabaya ya mitandao hii ndio imekuwa tatizo kubwa kwa vijana wengi hali inayosababisha upotevu wa muda bila kutambua madhara ya kushindwa kutumia muda wao vizuri kwa ajili ya mambo ya msingi.matumizi haya yamekuwa sababu ya maadili ya vijana kuendelea kushuka kitaaluma kila kukicha jambo ambalo linahatarisha uwepo wa Taifa lisilozingatia maadili siku za usoni.

Umefika wakati wa kila mzazi na mawakala wa makazi kuchukua hatua zinazostaili ili kuhakikisha swala zima la maadili kwa watoto, vijana na jamii nzima linazingatiwa.

Tags:
About Author: Geofrey Shao